Tuesday 10 November 2009

Real wang’ang’ana Ronaldo majeruhi, Madaktari wa Timu ya Taifa ya Ureno kumcheki!!!
Winga wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amelazimika kusafiri hadi kwao Ureno ili Madaktari wa Timu ya Taifa ya Ureno wampime baada ya Klabu yake kugoma na kudai hayuko fiti kucheza na inabidi apumzishwe wiki mbili zaidi.
Ronaldo amechaguliwa Timu ya Ureno ambayo inakabiliwa na mechi muhimu sana za Mtoano ili kuingia Fainali Kombe la Dunia hapo Jumamosi Novemba 14 na Jumatano Novemba 18 watakapocheza na Bosnia-Herzegovina na mshindi kwenye mechi hiyo ndio anaetinga Fainali Kombe la Dunia mwakani.
Ronaldo aliumia enka yake Septemba 30 kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE kati ya Real Madrid na Marseille na hajacheza mechi 7 kwa Klabu yake ingawa aliichezea Ureno Oktoba 10 walipocheza na Hungary kwenye mechi ya Makundi Kombe la Dunia na ndipo akajiumiza tena kwenye enka hiyo hiyo majeruhi.
Bosi wa Ureno, Carlos Queiroz, ambae aliwahi kuwa Meneja wa Real Madrid na pia Msaidizi wa Sir Alex Ferguson Manchester United, amesema: “Sheria za FIFA zinatulinda na hivyo tutampima. Tunaheshimu kila Klabu lakini hii ni haki yetu kuridhika kuhusu Mchezaji wetu.”
Bendtner kufanyiwa operesheni!!
Arsenal imethibitisha kuwa Mshambuliaji wao toka Denmark, Nicklas Bendtner, atafanyiwa upasuaji ili kumtibu nyonga na atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 4.
Bendtner aliumia Oktoba 31 Arsenal ilipowafunga Tottenham 3-0 kwenye Ligi Kuu Uwanjani Emirates.
Mshambuliaji huyo, alieifungia Arsenal goli 3 msimu huu katika mechi 13, atafanya hiyo operesheni huko Ujerumani.
Goli la mwisho alilofunga Bendtner ni lile lililowaua na kuwatoa Liverpool nje ya Kombe la Carling alipopachika bao la pili na kuwapa Arsenal ushindi wa 2-1. 
Liverpool: Uwanjani matokeo si mazuri, Wachezaji wazidi kujeruhiwa!!!
Ingawa Rafa Benitez amewapa faraja kidogo Wadau wa Liverpool pale alipotangaza Mhimili wao mkuu, Fernando Torres, halazimiki kufanyiwa upasuaji ili kutibu maumivu yake na pia Gerrard kuonekana uwanjani jana, lakini wasiwasi unazidi kutanda kwa matokeo ‘mabovu’ uwanjani na listi ya majeruhi kuongezeka kwa Wachezaji wanaotumainiwa.
Wachezaji Albert Riera na Yossi Benayoun waliocheza mechi ya jana Liverpool waliyotoka suluhu 2-2 na Birmingham walilazimika kutoka nje ya uwanja huku wakichechemea na Benitez amethibitisha itabidi wawe nje kwa muda pamoja na Mlinzi Dan Agger mwenye matatizo ya mgongo.

No comments:

Powered By Blogger