Sunday 8 November 2009

Fergie atimiza Miaka 23 Man U na kutoboa Klabu nyingi za nje zilimtaka!!
Sir Alex Ferguson ametoboa kuwa katika miaka yake 23 aliyotimiza Ijuma iliyopita Klabu nyingi kubwa za nje ya England zimekuwa zikimpa ofa nono ya kwenda kufundisha lakini mwenyewe amekiri “huwezi ukaikimbia Manchester United!”
Katika miaka hiyo 23 akiwa Old Trafford na Manchester United, Sir Alex Ferguson amefanikiwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 11, Ubingwa wa Ulaya mara 2, Kombe la FA mara 5, Kombe la Ligi mara 3, Kombe la Washindi Ulaya mara 1, Kombe Klabu Bingwa Duniani mara 2 na UEFA Super Cup mara 1.
Ferguson amekiri: “Nimepata ofa nyingi tu lakini hakuna hata moja iliyonivutia!”
LIVERPOOL HAIUZI MTU!!!
Mmojawapo wa Wamiliki wawili Liverpool, Tom Hicks, amewahakikishia Mashabiki wao kuwa hata kama Liverpool itatolewa mapema kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE wao hawana nia ya kuuza Mchezaji yeyote.
Msimu huu Liverpool wameuanza kwa balaa kwani wapo nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na pia wako hali mbaya kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE huku wakitakiwa washinde mechi zao zote 2 zilizobaki Kundini mwao na pia kuomba wengine wapate matokeo mabaya ili wao wasonge mbele.
Hali hii mbaya imefanya kuzagae habari kuwa Mastaa kama Fernando Torres na Steven Gerrard huenda wakang’oka na imebidi Mmiliki huyo Tom Hicks ajitokeze kutuliza watu.
Kipa wa Sunderland avunjika mkono!!
Sunderland imethibitisha kuwa Kipa Craig Gordon ambae pia huidakia Timu ya Taifa ya Scotland amevunjika mkono baada ya kuumizwa na Jermaine Defoe, Straika wa Tottenham, kwenye mechi ya Ligi Kuu jana ambayo Tottenham iliifunga Sunderland 2-0 uwanjani White Hart Lane.
Kipa huyo mwenye umri wa miaka 26 alitolewa na nafasi yake kushikwa na Marton Fulop.
Meneja wa Sunderland Steve Bruce amethibitisha kuumia kwa Gordon lakini hakusema atakuwa nje kwa muda gani.

No comments:

Powered By Blogger