Monday 9 November 2009

Fletcher: “Wenger ananiponza kwa Marefa!”

Darren Fletcher anaamini kabisa Marefa sasa wanamsakama mno kufuatia matamshi ya Meneja wa Arsenal Arsene Wenger,  mwanzoni mwa msimu, alipokuwa akinung’unika baada ya Arsenal kupigwa 2-1 na Manchester United kwenye mechi ya Ligi Kuu Uwanjani Old Trafford, na kudai Man U imecheza 'kinyume na soka' na Wachezaji wake kucheza rafu.
Ingawa baada ya mechi hiyo Wenger hakumtaja kwa jina Kiungo huyo wa Man U, lakini ilikuwa ‘siri ya wazi’ maneno yake hayo na hasa alipotamka kwamba kuna Mchezaji katika mechi hiyo alikuwa akicheza rafu mfululizo bila ya kuonywa na Refa yalimlenga Fletcher.
Fletcher amesema: “Kauli ya Bwana Wenger sasa inaanza kuwafanya Marefa waone mie ni Mchezaji mchafu! Ile frikiki iliyowapa goli Chelsea sio faulo! Sikucheza rafu, niliupiga mpira kwa kisigino na Cole akajirusha juu! Sasa tunaanza kuona madhara ya Wenger! Lakini itabidi tuipandishe soka yetu ili maamuzi haya mabovu yasituumize zaidi!”
Tangu msimu uliopita chati ya Darren Fletcher imepanda juu sana hapo Manchester United na sasa anaonekana ni Mchezaji muhimu sana.
Wadau wengi wanaamini kukosekana kwake kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, baada ya kupewa Kadi 'feki' kwenye Nusu Fainali ambazo Man U waliwapiga Arsenal nje ndani, ndiko kulisababisha Barcelona kushinda Fainali hiyo.

No comments:

Powered By Blogger