Saturday 28 August 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

MADAI SCHOLES ‘MCHEZA RAFU’, ROVERS ‘WACHEZA RAGA’: Fergie, Big Sam wajibu mapigo kwa Wenger!
• Mourinho nae amkandya!
Kufuatia Arsene Wenger kutoa shutuma kuwa Kiungo Veterani wa Manchester United, Paul Scholes, ni ‘Mcheza Rafu’ na Timu ya Blackburn Rovers ni ‘Wacheza Raga’, Mameneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, na wa Blackburn, Sam Allardyce, Big Sam, wamejibu mapigo.
Big Sam amedai Wenger amechanganyikiwa na sasa hata hajui afanye nini ili kushinda Vikombe.
Ferguson amenena Wenger ameonyesha kutokuwa na heshima kwa kumbandika Scholes sifa ambayo hastahili.
Leo, Arsenal itatinga Ewood Park, nyumbani kwa Blackburn Rovers, Timu ya Big Sam, ambayo Msimu uliokwisha iliwaliza Arsenal kwa bao 2-1 na mechi hiyo imemfanya Wenger aombe hifadhi ya Refa ili kuwanusuru Wachezaji wake wasikumbane na ‘Soka la Raga’.
Kihistoria, Wenger na Big Sam washakutana mara 21 na ni mara 8 tu ndizo Wenger ameshinda.
Big Sam amesema: “Hatustahili kuwafunga Arsenal lakini huwa tunawafunga. Si sababu ya Raga lakini mpaka pale watakaposema kwenye Soka usimguse mwenzio, soka ya ubavu ni muhimu!”
Big Sam akaongeza: “Hebu nimkumbushe Wenger. Timu yake ilikuwa ikuchukua Ubingwa na ndio ilikuwa Timu chafu kwa rafu kupita zote! Walikuwa Mabingwa huku wakiongoza kwa Kadi Nyekundu na Njano kupita Timu yeyote! Patrick Viera, Emmanuel Petit, Sol Campbell na Martin Keown walitumia kila mbinu chafu kushinda!”
Big Sam akachambua zaidi kwa kutamka: “Wenger amebadilisha mbinu. Ametoka kwenye Timu ile ya mibavu na uchafu na sasa Timu yake inatandaza Soka na kumuvu vizuri tu lakini wakati wote tunakubali Soka hilo linafurahisha kulitazama, lakini si Timu nzuri kama ile iliyopita iliyokuwa ikishinda Mataji kwa mibavu.”
Ni Miaka mitano sasa tangu Arsenal ishinde Kikombe pale iliposhinda FA Cup kwa matuta dhidi ya Manchester United.
Ingawa Miaka ya hivi karibuni uhusiano wa Wenger na Ferguson umeonekana poa na hata alipohojiwa Wenger akatania kuwa siku hizi Ferguson anamwona si tishio na ndio maana hawagombani, kauli ya Wenger kumsifia na papo hapo kumponda Scholes ni ‘Mcheza Rafu’ iliibua hisia Ferguson atalipuka.
Hata hivyo Ferguson alijibu tuhuma hizo kistaarabu kwa kusema: “Sijui kwa nini Wenger ametamka hilo. Najua Scholes si mzuri kwa kukaba Watu na mara nyingi hukosea na kuwavaa wenzake lakini hajamuumiza Mtu. Ni rahisi sana kusema ubaya wa Mchezaji yeyote! Naweza kusema hilo kuhusu Mchezaji wake mmoja wa Arsenal lakini sina haja. Inashangaza kumponda Mchezaji ambae ametoa mchango mkubwa kwa Soka ya Uingereza kwa Miaka 18!”
Huko Madrid, Jose Mourinho ameendeleza libeneke la kumponda Arsene Wenger ingawa hakumtaja kwa jina wakati alipohojiwa.
Mourinho alitamka: “Kama huchezi vizuri, hushindi. Ni upumbavu kudai ‘Tulicheza vizuri, lakini hatukushinda!’ Hao huwa wanadai ilikuwa bahati mbaya, tulimiliki mpira asilimia 90 au tumefungwa dakika ya mwisho au kwa frikiki! Mara nyingi nawaona Makocha hao wana akili kupita mie! Mie nikifungwa, siku zote najiuliza kosa liko wapi.”
Alipoulizwa kama majibu yake yanamlenga Wenger, Mourinho alisema: “Kuna Kocha mmoja Timu zake zimekuwa zikicheza Soka safi kwa Miaka 10 na Wachezaji wake siku zote ni Vijana chipukizi. Siku zote ni Timu changa isiyokua na isiyoshinda chochote! Kwangu mie huu ni wehu na upuuzi mkubwa!”

No comments:

Powered By Blogger