Sunday 20 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Mabingwa wa Dunia Italy ulimi nje!!
Leo Jumapili Juni 20 huko Uwanja wa Mbombela, Nelspruit, Mabingwa wa Dunia Italia wameenda sare 1-1 na New Zealand, Timu ambayo wengi hawakuipa nafasi yeyote, lakini ilichachamaa vibaya.
Hii ni sare ya pili kwa Italia baada ya kutoka droo mechi ya kwanza na Paraguay na sasa watamaliza mechi iliyobaki kwa kucheza na Slovakia.
New Zealand watacheza na Paraguay ambao ndio wanaongoza Kundi hili wakiwa na pointi 4.
Katika mechi ya pili sasa, Mabingwa hao wa Dunia walijikuta wako nyuma kwa bao 1-0 dakika ya 7 baada ya frikiki ya Shane Elliot kuparazwa kichwa na Reid na kumgonga Nahodha wa Italia Cannavaro kifuani na kumkuta Mfungaji Smeltz alieudokoa kumpita Kipa Marchetti.
Italia walicharuka baada ya kufungwa na kuishambulia New Zealand mfululizo na hatimaye presha yao ilizaa penalti dakika ya 28 baada ya Beki Tommy Smith kumshika jezi De Rossi ingawa ilionekana De Rossi alijirusha kuitafuta hiyo penalti.
Iaquinta akamchambua Kipa Paston na kufanya ngoma iwe 1-1.
Licha ya kutawala mechi Kipindi cha Pili, Italia walishindwa kupata bao la pili na kuna wakati ‘kaunta ataki’ ya Ne Zealand nusura iwape bao la pili.
Timu:
Italy: 12-Federico Marchetti; 19-Gianluca Zambrotta, 5-Fabio Cannavaro, 4-Giorgio Chiellini, 3-Domenico Criscito; 15-Claudio Marchisio, 22-Riccardo Montolivo, 6-Daniele De Rossi, 7-Simone Pepe; 9-Vincenzo Iaquinta; 11-Alberto Gilardino.
New Zealand: 1-Mark Paston; 4-Winston Reid, 19-Tommy Smith, 6-Ryan Nelsen; 11-Leo Bertos, 5-Ivan Vicelich; 7-Simon Elliot, 3-Tony Lochhead; 9-Shane Smeltz; 10-Chris Killen, 14-Rory Fallon.
Refa: Carlos Batres (Guatemala)
Ufaransa yasambaratika!!!
Kuna taarifa kuwa Timu ya Ufaransa leo mchana ilishindwa kufanya mazoezi baada ya kuzuka zogo kati ya Mkufunzi wa Mazoezi ya Viungo na Kocha wa Ufaransa, Raymond Domenech, na Wachezaji wote wakaondoka Uwanjani na kuingia ndani ya Basi lao.
Baada ya hapo zikaibuka habari kuwa Mkurugenzi wa Timu, Jean-Loius Valentin amejiuzulu kwa hasira.
Balaa lote hili limezuka baada ya Straika Nicolas Anelka kutimuliwa kwenye Timu baada ya kugombana na Kocha Domenech.
Hata hivyo Domenech amedai Anelka alipewa nafasi ya kubaki kwenye Timu ikiwa ataomba radhi lakini alikataa.
Kaita atishiwa maisha baada ya Kadi Nyekundu
Kiungo wa Nigeria, Sani Kaita, ambae alitolewa kwa Kadi Nyekundu Siku ya Alhamisi Ugiriki ilipoifunga Nigeria 2-1 kwenye Kombe la Dunia ameshapokea vitisho vingi vya maisha yake.
Msemaje wa Timu ya Nigeria, Peterside Idah, amesema Kaita ameletewa zaidi ya barua pepe 1,000 zinazotishia maisha yake toka kwao Nigeria.
Mseamaje huyo ameongeza kuwa washatoa taarifa kwa Serikali ya Nigeria na FIFA kuhusu matukio hayo ya vitisho.
Kaita alipewa Kadi Nyekundu baada ya kumrushia teke Vassillis Torosidis wa Ugiriki dakika ya 33 huku Nigeria wakiongoza 1-0 lakini wkicheza pungufu wakafungwa 2-1 na sasa nafasi yao ya kuendelea Raundi ya Pili ni finyu na pia ni lazima waifunge Timu ngumu Korea ya Kusini katika mechi ya mwisho Siku ya Jumanne ili wawe na matumaini.

No comments:

Powered By Blogger