Tuesday 22 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Sokomoko kambi ya England: Bifu Capello na Terry
Kufuatia mwendo wa kusuasua katika mechi zao mbili za awali ambazo zote wametoka sare na sasa inabidi waifunge Slovenia katika mechi yao ya mwisho ikiwa watataka kufuzu kuingia Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia, kumezuka mtafaruku mkubwa ndani ya Kambi ya England baada ya kwanza Nahodha wa zamani John Terry kujitokeza na kudai Wachezaji hawafurahii jinsi Timu inavyoendeshwa na Capello, kisha akatokea Capello mwenyewe akijibu mapigo na kusema Terry amefanya kosa kubwa kutoa madai yake.
England ilianza kampeni yake kwa sare na USA ya bao 1-1 kisha droo ya 0-0 na Algeria.
Kocha Fabio Capello amesema siku zote mlango wake uko wazi kwa Mchezaji yeyote kuongea nae na ameshangazwa na kauli za Terry kwenye kadamnasi.
Terry ndie alikuwa Nahodha wa kwanza chini ya Capello lakini alitimuliwa baada ya kupatwa na skandali ya kutembea na Gelfrendi wa Mchezaji mwenzake Wayne Bridge.
Hata hivyo, John Terry amejitokeza na kuomba msamaha kwa kusema kauli zake zilikuwa ni kutaka kufafanua ukweli na hakuwa na nia ya kumponda Capello.
Ingawa inaaminika Terry atacheza mechi hiyo ya mwisho ya Kundi C na Slovenia hapo Jumatano Juni 23 lakini inaonekana siku zake kuichezea England chini ya mamlaka ya Capello zimeanza kuhesabika.
Spain 2 Honduras 0
FIFA wasubiri ripoti ya Refa kuhusu Villa
Ingawa Spain jana Jumatatu Juni 21 waliifunga Honduras 2-0 na hivyo kujiongezea matumaini ya kuingia Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia huenda Straika wao wa kutumainiwa David Villa akawa matatani ikiwa Refa wa pambano hilo Yuichi Nishimura ataamua achukuliwe hatua kwa kosa la kumpiga Beki wa Honduras Emilio Izaguirre.
Villa alimpiga Beki huyo wakati wakisubiri frikiki ipigwe lakini Refa hakuchukuwa hatua yeyote wakati huo na sasa ataonyeshwa video ya tukio na atatakiwa aamue hatua ipi angechukua kama angeliliona tukio hilo.
Katika mechi hiyo, David Villa ndie aliefunga bao 2 za Spain na pia kukosa penalti aliyoipiga nje.

No comments:

Powered By Blogger