Wednesday 23 June 2010

FIKA: www.sokainbongo.com

Okocha alia, alaumu Afrika kwa uzembe!
Jay-Jay Okocha, Supastaa wa zamani wa Nigeria, amelalamika kuwa Soka la Afrika haliwezi kufanikiwa mpaka Watu wakae chini na kutafakari upya nini kifanyike ili tufanikiwe katika Fainali za Makombe ya Dunia yajayo.
Okocha, Miaka 36, ambae aliwahi kuwa Mchezaji Ligi Kuu England akiwa na Bolton Wanderers na kisha Hull City, amedai Afrika tunatumia njia za mkato za kujitayarisha na Mashindano yaliyo mbele yetu badala ya kuwekeza katika kutafuta, kukuza na kuendeleza vipaji vya Watoto na Wachezaji chipukizi.
Pia, amesema hatufanyi jitihada za kutosha za kuwaendeleza Makocha Wazalendo.
Okocha akawageukia Masupastaa wa leo wa Afrika wanaochezea Nchi zao huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kudai hawajaonyesha moyo thabiti wa kuchezea Nchi zao kama wanavyofanya wakiwa na Klabu zao huko Ulaya.
Okocha alilalama: “Hii ni hulka ya mtu. Wachezaji wetu hawakuonyesha ari ya kutosha. Haya Mashindano yako Afrika na tulidhani tutanufaika lakini sivyo!”
Mbali ya kubwagwa nje Cameroun, Algeria, Nigeria na Afrika Kusini, wakiwa Wenyeji wa kwanza wa Fainali za Kombe la Dunia kubwagwa nje Raundi ya Kwanza tu, tumebakiwa na Ivory Coast, wenye nafasi finyu, na Ghana pekee ndio kidogo wamegangamala.
Okocha alimaliza kwa kusema kwa msisitizo Afrika ni lazima ijifunze toka Ligi za juu za huko Ulaya na Watu wawe na nidhamu ya kuendesha Soka kitaaluma na sio kwa kulipua na ubabaishaji.

No comments:

Powered By Blogger