Friday 25 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Brazil, Ureno zaingia Raundi ya Pili!
Ivory Coast 3 North Korea 0
Brazil na Ureno zimetoka sare 0-0 na zote zimeweza kuingia Raundi ya Pili ya Mtoano ya Timu 16 ya Kombe la Dunia na watakutana na Timu toka Kundi H ambalo lina Chile, Spain, Honduras na Uswisi ambazo zinacheza baadae leo kuamua hatma ya Kundi hilo na nani atacheza na Brazil na Ureno.
Licha ya kuifunga North Korea 3-0, Ivory Coast imeyaaga mashindano
haya kwa kumaliza nafasi ya 3.
Hivyo, kwa Afrika, ni Ghana pekee ndio iko Raundi ya Pili.
RATIBA: Jumamosi Juni 26
Raundi ya Pili Mtoano wa Timu 16
[saa za bongo]
Saa 11 jioni: Uruguay v South Korea Nelson Mandela, Port Elizabeth
Saa 3.30: USA v Ghana Royal Bafokeng, Rustenburg
Dunga na Bifu lake na Mapaparazi wa Brazil
Timu ya Brazil siku zote huandamwa na kundi kubwa la Wanahabari popote wanapoenda na huko Afrika Kusini waliko kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia hali si tofauti.
Kuna Waandishi zaidi ya 700 wanaotoka Brazil kuifuatilia Timu yao.
Lakini safari hii, tofauti na miaka ya nyuma, kazi yao imekuwa ngumu mno kwani walikuwa wamezoea kuongea na Timu na Mchezaji yeyote wakati wowote wanaotaka lakini safari hii wamewekewa ngumu na Kocha wa Brazil Dunga ambae ameiondoa kabisa fursa hiyo na hivyo kuleta msuguano mkubwa kati yake na Wanahabari hao.
Dunga amewaamrisha Wachezaji kutoongea na Wanahabari na pia amewazuia kufika kwenye mazoezi na maamuzi hayo yamewastua na kuwakera Waandishi wa Habari.
Huko Ujerumani, kwenye Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2006, kundi la Wanahabari walikuwa na uhuru mkubwa wa kuongea na Wachezaji na ilifika siku Ronaldo na Roberto Carlos walihojiwa alfajiri ili wawe laivu kwenye TV kubwa huko kwao Brazil.
Baada ya Brazil kubwagwa nje ya Mashindano hayo yakaanza malalamiko toka kila upande kuwalaumu Wanahabari kwa kuwaandama Wachezaji masaa 24.
Ndipo alipoingia Dunga kama Kocha wa Brazil na kufutilia mbali hiyo sarakasi ya Wanahabari.
Huko Afrika Kusini, Brazil inaruhusu Waandishi kuongea na Wachezaji wawili tu kwa siku na mazoezi hufanywa bila ya Wanahabari kuwepo.
Hata Mashabiki wamezuiwa kwenda mazoezini na ni mara moja tu, kama FIFA inavyotaka, ndio mazoezi yalikuwa wazi kwa Waandishi na Mashabiki.
Hali hii imeleta manung’uniko makubwa toka kwa hao Waandishi kutoka Brazil lakini Dunga ameshikilia msimamo wake na amesema: “
Kuna Waandishi 300 toka Brazil wanangojea tu Selecao ifungwe!”
Katika mkutano mmoja na Wanahabari mara baada ya Brazil kuifunga Korea Kaskazini 2-1 katika mechi ya ufunguzi yao ya Kombe la Dunia, Dunga alizozana na mmoja wa Waandishi na akamwambia: “Mwaka jana, Robinho alipokuwa akichezea Manchester City, wengi hawakutaka achezee Brazil! Na wewe ulikuwa mmoja wao!”
Kuhusu kutoruhusu Wanahabari mazoezini, Dunga aliwaambia: “Nyie siku zote mnalalamika Wachezaji sio wabunifu sasa kama humuoni mazoezi basi kuweni wabunifu na mtunge stori zenu!”
Ballack ajiunga Bayer Leverkusen
Kiungo wa zamani wa Chelsea Michael Ballack amerudi kwao Ujerumani na kujiunga na Klabu aliyowahi kuichezea zamani Bayer Leverkusen kwa mkataba wa Miaka miwili.
Ballack, Miaka 33, ambae amezikosa Fainali za Kombe la Dunia kwa kuumia, hakuongezewa Mkataba na Chelsea na hivyo amejiunga Bayer Leverkusen kama Mchezaji huru.
Ballack aliwahi kuichezea Bayer Leverkusen kati ya 1999 na 2002 na alifika nayo Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI Mwaka 2002.
Kisha akahamia Bayern Munich hadi Mwaka 2006 alipojiunga na Chelsea.

No comments:

Powered By Blogger